Hits 40644 | 1 online
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Haroun Ali Suleiman amesema hajafurahishwa na kasi ndogo ya ujenzi wa jengo la Mahakama kuu unaoendelea Tunguu na kukerwa na visingizio vya athari za ugonjwa wa corona na tatizo la uhaba wa mchanga katika kukamilisha miradi ya Serikali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Haroun Ali Suleiman amesema hajafurahishwa na kasi ndogo ya ujenzi wa jengo la Mahakama kuu unaoendelea Tunguu na kukerwa na visingizio vya athari za ugonjwa wa corona na tatizo la uhaba wa mchanga katika kukamilisha miradi ya Serikali.
Akizungumza na watendaji wa Mahakama kuu ya Zanzibar wakiongozwa na Jaji mkuu Omar Othman Makungu, alisema haipendezi hata kidogo kuona ujenzi wa mradi wa jengo la kisasa la Mahakama kuu limeshindwa kukamilika katika kipindi cha uongozi wa Rais wa awamu ya 7 Dkt.Ali Mohamed Shein ambaye ndiye aliyeanzisha mradi huo wenye lengo la kuhakikisha Zanzibar inakuwa na majengo ya kisasa ya Mahakama.
Alisema visingizo vya wakandarasi wa mradi huo ambao ulikuwa ukabidhiwe Serikalini Oktoba 2020 mwaka huu havikubaliki kwani suala la mchanga halimo katika makubaliano ya mkandarasi na serikali.
''Nimesikitishwa na kuchelewa kukamilika kwa mradi huu na sijaridhishwa visingizio vilivyotolewa na mkandarasi havikubali....suala la mchanga ni jukumu la mkandarasi na sio Serikali na ugonjwa wa corona isiwe kisingizio cha kutokamilika kwa mradi naomba mfahamu Serikali itasaidia pale inapohitajika kwani ni jukumu letu kuona miradi yote inakamilika kwa wakati’.
Mhe Waziri alisema Serikali imechukuwa uamuzi wa kujenga jengo jipya na la kisasa la Mahakama Kuu kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kupata nafasi nzuri ya kusikilizwa kwa mashauri yao ili watendaji wakiwemo Majaji na Mahakimu waweze kuendesha kesi kwa faragha zaidi.
Aidha alitoa maelekezo wa mkandarasi huyo kuhakikisha mradi huo unakamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi wa Disemba kwa kuzingatia viwango na ubora wake kwa ujumla na kutolea mfano wa jengo la Mahakama Kuu iliyopo Vuga ambalo limedumu zaidi ya miaka 100 .
Mapema Mtendaji Mkuu wa Mahakama kuu ya Zanzibar Ndg Kai Bashir Mbarak amesema miongoni mwa sababu zilizopelekea kwa mkandarasi wa mradi huoambae ni kampuni ya Advert Construction kuchelewa kukamilisha kazi kwa wakati ni kuwepo kwa tatizo kubwa la uhaba wa mchanga .
Kwa mfano alisema wamekuwa wakipata tani 100 za mchanga kwa wiki sawa na gari kumi ambazo hazitoshelezi mahitaji ya mradi huo mkubwa na hali hiyo ni baada ya kufanyika kwa mazungumzo kati ya Mahakama na Wizara ya kilimo maliasili.
Aidha alizitaja sababu nyengine ikiwemo kuzuka kwa ugonjwa corona ambao umepelekea baadhi ya vifaa kushindwa kuwasili nchini kwa wakati kutoka nje ya nchi.
''Baadhi ya vifaa ikiwemo madirisha ndiyo vimewasili nchini juzi.....tatizo kubwa ni kuzuka kwa ugonjwa wa corona ambao bado unaendelea kuisumbuwa dunia hadi sasa''alisema.
Ujenzi wa jengo la Mahakama kuu ya Zanzibar liliopo Tunguu unagharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa asilimia mia moja huku jumla ya sh. sh.Bilioni 16 zikitengwa kwa ajili ya kusimamia mradi huo.
Awali Mhe Haroun alifanya mazungumzo na Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe Omar Othman Makungu ofisini kwake Vuga na kujadili mambo mbali mbali yenye lengo la kuleta ufanisi katika utendaji wa kazi kwa kuchukia yale yote yanayoweza kuleta athari za kiutendaji, kuziba mianya ya rushwa, kuhakikisha wanatenda haki katika hukumu za kesi zikiwemo za udhalilishaji ambazo zinalalamikiwa sana pamoja na kuangalia maslahi ya watendaji
Pia Waziri Haroun alisisitiza kuyafanyia kazi maagizo na maelezo yote aliyoyatoa Mhe Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dkt Hussein Ali Mwinyi wakati wa kuwaapisha Mawaziri na kusema kuwa yalikuwa ni maagizo kwa watendaji wote hivyo ni lazima kuwatumikia wananchi vizuri kila mmoja awajibike kwa kufanya kazi kwa uadilifu
Nae Jaji Mkuu Mhe Omar Othman Makungu amempongeza Mhe Haroun na kuahidi kuendeleza uwaminifu, uwajibikaji, uadilifu, nidhamu maadili mema kwa kila mtendaji wa mhimili wa mahakama